Jumapili 28 Juni 2026 - 16:53
Wahalifu wa kivita wa Minab na Lamerd wanapaswa kufikishwa kwenye vyombo vya mahakama vya ndani na vya kimataifa

Hawza/ Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi nchini Iran, amesema katika ujumbe wake kufuatia mnasaba wa Wiki ya Mahakama kwamba: Kuanzia damu ya mashahidi madhalimu wa vita vya pili na vya tatu vya kulazimishwa, hadi majeraha na madhara ya kimwili, kisaikolojia, kimali na kiroho yaliyolikumba taifa letu pendwa na kila mmoja wa wananchi wanyonge wa Iran ndani na hata nje ya nchi; kuanzia mauaji ya watoto nchini Minab na Lamerd na uhalifu wa kivita usio na mfano, hadi mashambulizi dhidi ya vituo vya tiba na huduma; kuanzia mauaji ya watoto wachanga wa siku chache hadi wazee wetu wapendwa; na juu ya yote hayo, kuuawa kishahidi kwa shakhsia ya kipekee, lulu isiyo na mfano na wa pekee wa zama hizi, kiongozi mkubwa wa jihadi, Mwenyezi Mungu auinue zaidi daraja lake tukufu, kila moja ya matukio haya linaunda jalada moja kati ya mamia, bali maelfu ya mashauri muhimu ya kisheria ambayo yanapaswa kufuatiliwa kwa uzito katika mahakama za ndani na za kimataifa.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza kutoka Tehran, umechapishwa ujumbe wa Ayatullah Sayyid Mujtaba Husseini Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi, kwa mnasaba wa Wiki ya Mahakama na kumbukumbu ya mwaka wa kuuawa kishahidi Ayatullah Beheshti pamoja na wenzake.

Matini kamili ya ujumbe wake ni kama ifuatavyo:

Kwa Jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, Mwenye Kurehemu

Natoa mkono wa pole kwa wananchi wote wa Iran na Umma wa Kiislamu kwa mnasaba wa siku za msiba wa Aali wa Mwenyezi Mungu na kuuawa kishahidi Imam Hussein (as), pamoja na wafuasi wake waaminifu.

Harakati na mapinduzi ya Imam Hussein (as) kwa ajili ya kusimamisha haki, kuufanyia mageuzi Umma na kupambana na dhuluma na uonevu ni kilele cha historia katika mapambano kati ya haki na batili, uadilifu na dhuluma, na inatoa mafunzo yenye thamani kubwa na yasiyosahaulika kwa watu wote huru duniani.

Damu ya Bwana wa Mashahidi, Imam Hussein (as), huitwa damu ya Mwenyezi Mungu, ambayo hutiririka katika mishipa ya ulimwengu na kuumba mashujaa na harakati zinazotoa uhai. Mapinduzi na Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kwa kuwa ni tawi lililotokana na chemchemi hiyo yenye nuru, yanapaswa daima kujitahidi kufikia malengo ya mapinduzi ya Imam Hussein (as).

Tarehe saba Tir ya kila mwaka ni kumbukizi ya shakhsia mashuhuri ya Mapinduzi na mtu ambaye alipokuwa mkuu wa Idara ya Mahakama alifanya juhudi zisizokoma katika njia hiyo, hadi pale yeye pamoja na kundi la wenzake waaminifu wa Mapinduzi walipoonja utamu wa shahada. Kudhulumiwa kwake pamoja na mashahidi sabini na mbili waliokuwa pamoja naye kulithibitisha kuwa mfumo huu na waasisi wake vina sura ya Hussein (as).

Mafanikio ya Idara ya Mahakama yataimarisha imani ya wananchi kwa mfumo

Hadhi ya Idara ya Mahakama katika Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni kulinda haki za wananchi, kurejesha haki za umma na uhuru halali, kupambana na ufisadi, kutekeleza uadilifu, kusimamisha mipaka ya Mwenyezi Mungu na kusimamia utekelezaji wa sheria.

Matunda ya mafanikio katika njia hii, mbali na kupata radhi za Mwenyezi Mungu, ni kuimarika kwa imani ya wananchi kwa nguzo hii ya mfumo. Matarajio ya haki kutoka kwa mihimili yote ya dola, taasisi na vyombo vinavyohusika ni kwamba daima virekebishe na kupanga upya utendaji wao kwa kuzingatia viwango vinavyotakiwa na Mfumo Mtukufu wa Jamhuri ya Kiislamu na hadhi ya juu ya taifa.

Katika jambo hili, Idara ya Mahakama ina nafasi ya kipekee, isiyo na mfano, katika kurekebisha mwenendo wa mambo na kuhamasisha sekta nyingine za mfumo. Hili linahitaji kuendelezwa kwa mchakato wa mageuzi na ujenzi mpya ndani ya idara hiyo yenyewe.

Kwa sasa matarajio ya jumla ya watu ni kuona msisitizo wa kivitendo juu ya jambo hili katika utendaji wa Idara ya Mahakama.

Kwa namna ambayo mageuzi ya mahakama hayatabaki kuwa maneno yaliyoandikwa katika hati za mageuzi na mipango ya utekelezaji, bali yatageuka kuwa uhalisia unaoonekana katika nyanja zote husika; kuanzia ofisi za majengo ya mahakama na vikao vya kesi hadi katika mazingira ya umma na maisha ya kijamii. Hali hiyo iweze kuwafanya wananchi waone athari zake chanya katika maisha yao ya kila siku kupitia uthabiti wa kupambana na aina zote za ufisadi, kupungua kwa ukiukwaji wa haki, kuharakishwa kwa usikilizaji wa mashauri, kuongezeka kwa uadilifu na ubora wa maamuzi ya majaji, pamoja na urahisi zaidi wa kupata viwango vya haki.

Kufuatilia haki zilizoporwa za taifa la Iran kutokana na uhalifu wa kimataifa wa miaka 1404 na 1405 ni miongoni mwa masuala muhimu zaidi ya kimahakama nchini

Katika taswira hii ya Idara ya Mahakama, utekelezaji wa haki unapaswa kufikia kiwango ambacho kila mwenye kudhulumiwa aione kuwa ni mahali pake pa kupata hifadhi. Hususan wale wenye aina yoyote ya madaraka wasiwe na ujasiri wa kukiuka haki za wengine, na mlango wa upendeleo na mapendekezo ufungwe kabisa, kiasi kwamba kuwa na mtu wa kufahamiana katika baadhi ya sehemu za idara hiyo kusiwe na manufaa yoyote.

Bila shaka, kurejesha haki za taifa hakuhusiani tu na masuala ya watu binafsi, haki zote za umma na za kijamii, kuanzia haki ya usalama wa kiuchumi na upatikanaji wa fursa kwa usawa, hadi haki ya kunufaika kwa haki na neema za kiasili, mazingira safi, uhuru halali na utawala wenye ufanisi, vyote ni miongoni mwa masuala muhimu katika kueneza uadilifu.

Miongoni mwa masuala muhimu zaidi ya kisheria na kimahakama yanayolihusu taifa lote la Iran katika kipindi hiki ni kufuatilia na kurejesha haki zao zilizoporwa kutokana na uhalifu wa wahalifu wa kimataifa, mabeberu na wavamizi wa kimataifa, hususan katika miaka ya 1404 na 1405.

Ni lazima wahalifu wa kivita wa Minab na Lamerd wafikishwe kwenye vyombo vya mahakama vya ndani na vya kimataifa

Kuanzia damu ya mashahidi waliodhulumiwa wa vita vya pili na vya tatu vya kulazimishwa, hadi majeraha na madhara ya kimwili, kisaikolojia, kimali na kiroho yaliyolipata taifa letu pendwa na kila mmoja wa wananchi wanyonge wa Iran, ndani na hata nje ya nchi; kuanzia mauaji ya watoto na uhalifu wa kivita usio na mfano huko Minab na Lamerd, hadi mashambulizi dhidi ya vituo vya tiba na huduma; kuanzia mauaji ya watoto wachanga wa siku chache hadi wazee wetu wapendwa; na juu ya yote hayo, kuuawa kkshahidi shakhsia ya kipekee isiyo na mfano, johari isiyo na kifani na mtu wa pekee wa zama hizi, kiongozi mkubwa wa jihadi – Mwenyezi Mungu auinue zaidi daraja lake tukufu – kila moja ya matukio haya linaunda jalada moja kati ya mamia, bali maelfu ya mashauri muhimu ya kisheria ambayo yanapaswa kufuatiliwa kwa uzito katika mahakama za ndani na za kimataifa.

Jambo lililo wazi ni kwamba; ni lazima wahalifu washikwe na wapatiwe adhabu inayostahili kutokana na uhalifu wao. Hoja muhimu katika suala hili ni kwamba, kwanza, kukiri na hata kujivunia kwa fedheha kulikofanywa na baadhi ya viongozi wa maadui wa Kimarekani na Kizayuni kuhusu uhalifu huu, bila shaka kunahesabiwa kuwa ni kukiri kutenda jinai, na jambo hilo limeandaa kwa namna inayofaa msingi wa kurejesha haki zilizoporwa za taifa.

Pili, kutekeleza kwa uzito maelekezo ya Kiongozi Shahidi wa Mapinduzi aliyoyatoa katika mkutano wake wa mwisho na viongozi wa Idara ya Mahakama mwezi Tir Shamia, mwaka uliopita kuhusu kushughulikia uhalifu uliotendwa katika vita vya pili vya kulazimishwa, kunahitaji pia kuyapanua maelekezo hayo ili yajumuishe vita vya tatu vya kulazimishwa, pamoja na kuendelea kuyafuatilia bila kukoma hadi kutolewa kwa hukumu na kukabidhi utekelezaji wake kwa watu wanaostahili. Hatua hii, kwa upande wake, itazuia kurudiwa kwa uhalifu wa aina hii.

Kuzingatia misisitizo ya Kiongozi Shahidi wa Mapinduzi ndiyo ufunguo wa mafanikio ya Idara ya Mahakama

Bila shaka, ili kufanikiwa katika njia ya mageuzi ya kina ya mfumo wa mahakama na kuongeza kasi ya kufikia malengo yaliyotajwa, kunahitajika maandalizi na masharti mbalimbali, mambo hayo kwa kiasi kikubwa yamekuwa yakielezwa mara kwa mara katika mikutano ya kila mwaka ya viongozi wa Idara ya Mahakama pamoja na nasaha na misisitizo ya kina ya Kiongozi Mkuu Shahidi wa Mapinduzi – Mwenyezi Mungu autakase moyo wake mtukufu. Kuzingatia kwa dhati maelekezo hayo na kujitahidi kuyatekeleza, jambo ambalo linahesabiwa kuwa ufunguo wa mafanikio ya viongozi waheshimiwa wa Idara ya Mahakama, ndilo ninalolisistiza na kulidai kwa uzito.

Njia ya kufikia uadilifu na kupambana na dhuluma pamoja na ufisadi ni njia ngumu, lakini itarahisishwa kwa ikhlasi na kumtegemea Mwenyezi Mungu, kushikamana na uchamungu wa kiwango cha juu, kuwa na hamasa na azma ya kweli, kufanya juhudi na bidii maradufu, kuwa na ujasiri na msimamo thabiti, kuwa na ubunifu katika utendaji, pamoja na kutumia kwa usahihi teknolojia za kisasa na kuendeleza mifumo ya kiakili (smart systems).

Kwa idhini ya Mwenyezi Mungu, kutimia kwa yote hayo kutawezekana chini ya kivuli cha rehema na uangalizi wa Bwana wetu, Mwenye Kusubiriwa, Msimamishaji wa Uadilifu, Imam Mahdi (as) – Mwenyezi Mungu aharakishe kudhihiri kwake – Inshaallah.

Sayyid Mujtaba Husseini Khamenei

7 Tir 1405 H.Sh. / 28 Juni 2026

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha